TUWASILIANE KWA E-mail: mobinsons@yahoo.com.

Sunday, November 25, 2007

Benedicto Mutungirehi: Mimi ni mbunge likizoni

Mobini Sarya
UKIANZA kuzungumza naye mara moja unagundua kuwa ni mwanasiasa mwenye mtazamo wa kidini zaidi kuliko siasa yenyewe. Anapokuwa katika jukwaa la siasa anakuwa tofauti na anavyoonekana.
Nilipokutana naye kwa mara ya kwanza tukiwa safarini Kigoma, nilidhani anasumbuliwa na jambo fulani la kusikitisha, kwani mara nyingi alikuwa kimya, hali iliyonilazimu kuchukua hatua ya kumfahamu zaidi.


Huyo si mwingine bali ni mbunge wa zamani wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Jimbo la Kyerwa, Benedicto Mutungirehi (40). Anasema kuwa hakushindwa ubunge bali amepumzika kwa muda yaani sawa na ‘mbunge aliyeko likizoni.’

Tangu ajiunge na siasa kwa mara ya kwanza mwaka 2000 na kugombea ubunge kupitia TLP Jimbo la Kyerwa, mkoani Kagera, amejipatia umaarufu nje na ndani ya jimbo lake, hasa baada ya kupata ushindi uliowashangaza wengi alipomwangusha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Eustace Katagira (CCM).

Umahiri wake wa kujenga hoja na kukwepa mtego wa kufungiwa ubunge, ulimjengea sifa nje na ndani ya Bunge hata kusababisha aliyekuwa Spika wakati huo, Pius Msekwa, kumpenda na kumpa nafasi kila wakati ya kusimama na kuchangia au kutoa hoja zenye ‘afya’ bungeni.

Lakini pia anasema umahiri wake wa kujenga hoja ulimwezesha kukwepa misukosuko wanayoipata wabunge wa upinzani, hadi kupendwa na Spika Msekwa na akawa anapewa mialiko ya nje.

Mutungirehi ametokea wapi?

Alizaliwa Mwaka 1967 katika kijiji cha Kitwe, wilayani Karagwe, akiwa mtoto wa nane katika familia ya mzee Mutungirehi.

Akiwa anasoma Darasa la Nne mwaka 1980, karama ya uongozi ilianza kujionyesha kuwa ni kiongozi alipogombea ukiranja mkuu alipopambana na mwanafunzi wa Darasa la Sita aliyekuwa amerudia shule. Alimshinda kwa kura nyingi.

Hapo ndipo karama ya uongozi ilipoanza kwani akiwa katika Shule ya Sekondari Kihororo Mwaka 1985 akiwa kidato cha pili, alichaguliwa kuwa mwenyekiti (Kaka Mkuu) wa serikali ya wanafunzi. Alipokuwa Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari ya Mirambo, Tabora, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa nidhamu.

Unaweza kusema ni mtu aliyezaliwa akiwa na karama ya uongozi, kwani alipojiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, sehemu ya Mlimani, akiwa mwaka wa pili mwaka 1994, alichaguliwa kuwa Rais wa serikali ya wanafunzi (DARUSO). Ndiye aliyekomesha tabia ya mapinduzi ya uongozi chuoni hapo.

Hata hivyo Mutungirehi anasema hatasahau jinsi alivyotaka kuuawa wakati anajaribu kuzima mapinduzi chuoni hapo. Anasema wapinduaji walikuwa wamejipanga kuitisha mkutano haramu na kumwekea mtego kuwa akifika tu ukumbini, waanzishe vurumai wapate nafasi ya kumuua.

Lakini alibahatika na kudokezwa na mtu asihudhurie huo mkutano atauawa. Alikini alifanya ukaidi, akaenda, kweli vijana wa Mlimani wakataka kumshambulia.

Anasema wakati wanataka kumpiga, alianguka chini akawa anarusha mateke. Kuona vile wale vijana wakakimbia wakidhani amekufa.

Chanzo cha mgogoro huo kilitokana na msimamo wake wa kutaka serikali iwakopeshe wanafunzi pesa za matumizi badala ya mzigo huo kukabidhiwa wazazi, lakini wanafunzi wao wakataka serikali ilipe gharama zote bila masharti, jambo analosema lisingewezekana na utaratibu wake ndio unaotumika hadi leo.

Kutokana na mgogoro huo, wakamtaka aondoke madarakani, uongozi wa chuo ukaingilia kati ukiwataka waitishe mkutano wamtoe kwa njia ya kidemokrasia ikashindikana. Chuo kikafungwa kwa miezi miwili huku wanafunzi wa kitengo cha uhandisi waliokuwa vinara wa mapinduzi wakasimamishwa mwaka mmoja.

Hata hivyo anajivunia kuwa wakati wake aliweza kufanya mambo makubwa ambayo leo hii yanatumika baada ya kufanikiwa kuingia Ikulu kuonana na Rais Ali Hassan Mwinyi akiwa na madai sita. Yote yalikubaliwa.

Moja ya madai hayo ilikuwa kama mtu ameajiriwa serikalini na akitaka kwenda kuongeza elimu chuo kikuu, alipwe mshahara badala ya utaratibu wa serikali uliokuwa unamzuia kulipwa bila kujali kama ana familia.

Pia alitaka sh 50,000 za kununulia vitabu wanafunzi zilizokuwa zinatumwa moja kwa moja kwenye duka la vitabu la chuo, wapewe pesa hizo wanunue wenyewe mitaani.

Tatu ilikuwa imetangazwa kuwa kwa mwanafunzi ambaye haendi likizo akibaki chuoni alipie chumba, wakapinga madai hayo wakataka akae bure. Pia serikali ilibadili mitaala ghafla ikasema anayesomea ualimu atakuwa anasoma miaka minne baadala ya mitatu, wakasema lazima ibaki mitatu. Pia waliiomba serikali ibadili matazamo ifungue milango ya majadiliano linapotokea tatizo la wanafunzi badala ya kufunga chuo.

Madai yote yalikubaliwa na serikali baada ya Rais Mwinyi akiwa na Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, wakati huo, Benjamin Mkapa, kuyapitia madai yao kwa kina.

Hayo ndiyo mafanikio anayojivunia kuyaacha Mlimani na uzoefu wa kiuongozi. Anasema kutokana na hayo, ameweza kujua namna ya kukabili tatizo anapokuwa anaongoza jumuiya ya watu wengi na kutoa maamuzi magumu.

Itikadi yake ilikuwa nini?
Wakati akiwa chuo kikuu akichukua shahada ya Sanaa na Lugha, alikuwa mfuasi mzuri wa Siasa za Karl Max na Lenin. Hakuwahi kuamini kama Mungu alikuwapo pamoja na kwamba alipokuwa mdogo alikuwa akipelekwa kanisani (Roman Catholic) na kaka yake alikobatizwa. Lakini jambo la kushangaza hakurudi tena kanisani.

Alikuwa haamini kama kuna shetani au nguvu yoyote ya giza. Alikuwa miongoni mwa wale wanaoamini kuwa historia ndiyo inayoongoza dunia na mtu huwa maskini kwa sababu mwenzake anamiliki mali zote, jambo lililomweka mbali na imani za kidini.

Mutungirehi alihitimu masomo yake ya chuo kikuu mwaka 1995 na kuamua kurudi kijijini kwao kulima badala ya kutafuta ajira nyingine akihofia kutoa au kupokea rushwa.

Pamoja na kuwa alitunukiwa Shahada ya Sanaa na Lugha mwaka 1995, lakini alikataa kuomba ajira kwa madai kuwa alihofia hangekwepa kupokea rushwa kutokana na mishahara ya wafanyakazi kipindi kile kuwa midogo kuweza kukidhi mahitaji.

Akiwa kijijini kwao, alichaguliwa kuongoza Chama cha Wakulima wa Kahawa cha chama cha ushirika - Karagwe Development Co-operative Union (KDCU) akiwa makamu mwenyekiti.

Hata hivyo hakudumu katika uongozi huo. Alilazimika kujiuzulu baada ya kuwashauri wanaushirika wa KDCU kuwa hafurahishwi na jinsi wanavyokiendesha chama hicho kwani kitawaletea wakulima hasara. Ukweli ulikuja kudhihirika baada ya kujiuzulu. Chama kilipata hasara kubwa aliyokuja kuitetea bungeni baada ya kuwa mbunge.

Anasema uongozi ndani wa chama hicho cha ushirika ulimsaidia sana wakati anagombea ubunge. Hakupata shida ya kushinda. Wanakaragwe walikuwa wanaufahamu mchango wake katika kuinua na kutetea soko la kahawa akiwa na kaulimbiu yake ‘Wakulima waachiwe wachague wenyewe soko la kuuzia kahawa.’

Alianza lini siasa?

Mwaka 2000 aliibuka ghafla kwenye siasa akijitokeza kugombea nafasi ya ubunge wa Jimbo la Kyerwa kupitia chama cha TLP. Chama hicho hakikuwa na umaarufu wala wafuasi wengi katika eneo hilo, lakini aliwashangaza wengi alipomwangusha aliyekuwa mbunge wa siku nyingi, Eustace Kataragira (CCM).

Alikuwa mbunge wa jimbo lake kwa kipindi kimoja tu cha miaka mitano, mwaka 2005 alipokujashindwa na Katagira kwa tofauti ya kura 2,800 uchaguzi anaosema ulijaa udanganyifu na wizi wa kura.

Lakini hakukata rufaa kwa sababu kesi nyingi huchelewa kuamuliwa.

“Mimi ninaamini uongozi hutoka kwa Mungu na Mungu anasema usiibe, sasa aliyeiba kura akakalia kiti kisicho chake atapata adhabu pamoja na waliomsaidia. Adhabu hiyo haiko mbali. Itakuwa fundisho kwake na kwa wengine wenye tabia hiyo,” anaonya Mutungirehi, sasa muumini wa Kanisa la Tanzania Asemblies of God (TAG).

Anasema alianza kwenda kanisani Oktoba 2006 katika Kanisa la Katoliki baada ya kuuasi ukomunisti, lakini Desemba mwaka huo alibadili madhehebu ghafla na kuhamia TAG kwa madai kuwa alipokea wito wa kumtaka abadili imani.

Mutungirehi anasema kwa kipindi alichokaa nje ya Bunge, amepata muda wa kupumzika na kufanya kazi yake vema ya ukatibu mwenezi wa TLP, nafasi aliyoipata Machi, mwaka huu.

Amewezaje kudumu TLP?

Anasema kuwa watu wengi wamekuwa wakimhoji amewezaje kuvumilia kuwako TLP ambako wengine wamekimbia.

Anaasema “Migogoro mingi katika vyama vya siasa inatokana na tamaa ya madaraka. Viongozi wengi wamekuwa wakishinikizwa kuachia madaraka wakati wao wanakuwa hawajaamua”.

Anasema hali hiyo husababisha vurugu na ndicho kisa cha wanachama wengi kuikimbia TLP, kwani walikuwa wanataka kumwondoa Mwenyekiti wa chama hicho, Augustine Mrema, bila kufuata utaratibu.

Yeye anasema yupo TLP kwa raha kwa vile hana haja ya kugombea madaraka na ndiyo maana watu wengi wamekuwa wakishindwa kumwelewa, kwani pamoja na kuwa na uwezo mkubwa kisiasa na kielimu ameendelea kubaki TLP pamoja na kwamba makada wa vyama vingine wamekuwa wakimshawishi ajiunge navyo.

“Kutaka aliyepo madarakani atoke ili wewe uingie ndiyo chanzo cha migogoro mingi inayosababishwa na tamaa ya madaraka. Mimi siwezi kufanya kosa la kuzurura kwenye vyama,” anasema na kuongeza kuwa anachoamini si kwa utashi wake, kama ambavyo wanasiasa wengine wanavyojiapisha kuwa hawawezi kuhama chama halafu baada ya muda mfupi wanahama.

Mutungirehi na ubunge

Akiwa mbunge alitetea bei ya soko la kahawa hadi serikali ikasikia kilio chake na kupandisha bei kwa asilimia 100. Alitumia muda mwingi baada ya Bunge kutembelea wapiga kura wake akiwaambia haki zao. Jambo hilo lilimjengea umaarufu mkubwa.

Wananchi wa Karagwe walikuwa wamedhulumiwa sh. bilioni 2 za baada ya kuuza kahawa. Akawapigania kwa kujenga hoja hadi wakapewa na amekuwa akitumia muda mwingi kuwaelimisha wakulima jinsi ya kuondokana na umasikini.

Anamzungumziaje Rais Kikwete?

Katika maoni yake kuhusu utawala wa Rais Jakaya Kikwete, anaonekana kuungana na Mchungaji Christopher Mtikila pale anaposema kuwa Rais Kikwete aliingia madarakani ‘kiharamu’ ingawa kwa macho ya kibindamu na kidemokrasia anaonekana kuwa alishinda.

“Kikwete alitumia njia mbaya kuingia Ikulu, amemchukiza Mwenyezi Mungu. Jambo hili atakuja kulijutia wakati atakapokuwa anapokea malipo yake muda si mrefu,” anasema mwanasiasa huyo, kama vile anatabiri kuwa katika nafasi nzuri ya kumrithi Mrema mara atakapostaafu.

Mutungirehi anasema kuwa hata hili vuguvugu la kisiasa linaloendelea hapa nchini, ni sababu ya hizo hizo kama dalili na ishara za mambo makubwa yanayokuja. “Ukimwona mbunge anayewakilisha wananchi amechomewa nyumba yake, vibaka wanauawa hovyo…ujue uongozi wa CCM unakwenda kuvunjika na mfumo mpya unaojali wananchi utasimama punde si punde,” anasema.

Mutungirehi anasema kuwa mfumo huo anaoutabiri utawekwa kwa makusudi na Mwenyezi Mungu ili kuondoa rushwa na kulinda maliasili za taifa hili zitumike kikamilifu na ufisadi uishe kabisa nchini.

Anaendelea kusisitiza kuwa Kikwete aliingia kwa njia mbaya, sasa ameanza kulipa gharama ndiyo maana anazurura nje badala ya kukaa ajenge uchumi wa nchi unaoporomoka kila siku.

Kuhusu uchumi, Mutungirehi anahoji uhalali wa serikali kuuza kila kitu - viwanda na mabenki - badala ya kujenga kama alivyokuwa anafanya mwasisi wa taifa hili, Mwalimu Julias Nyerere.

“Kama Nyerere asingejenga mabenki, reli na viwanda leo hawa wangekuwa wanauza nini? Hata ranchi ambazo Mwalimu Nyerere alikuwa anatengeneza wameuza, sasa vya kwao wanavyojenga viko wapi?” anahoji mwanasiasa huyo.

Anasema kuwa ili nchi iimarike kiuchumi, lazima mfumo wa ‘home-grown’ uimarike na ikitokea uchumi wa dunia umeharibika tujitegemee. Lakini hapa kwetu hakuna kitu kama hicho.

“Vipo vitu ambavyo serikali inapaswa kuwekeza ili kulinda uchumi wa nchi,” anashauri.

Anasema serikali imekuwa ikijinadi kuwa makusanyo ya kodi yanaongezeka, lakini bila kuangalia kuwa vyanzo vya mapato navyo vimeongezeka au ni mzigo unaongezeka kwenye vyanzo vilivyoopo.

“Serikali inaongeza kodi wao wanasema kwamba kodi imeongezeka na uchumi lakini hatuoni vitegauchumi vinaongezeka bali wanazidi kudidimiza vilivyopo, kwani kuongeza kodi ni uharibifu unaodidimiza kipato cha wananchi.

“Tatizo ni kwamba wanapenda kufanya mambo yao kisiasa, wakitaja mapato mengi wanapigiwa makofi lakini hawaangalii je, mwaka huu tumezalisha kama bidhaa tani ngapi na mwaka kesho itakuwa ngapi?” anahoji.

Anasema Rais Kikwete anakwepa kusoma takwimu za uchumi ili apate nafasi ya kukaa na wasomi, wamshauri namna ya kujenga uchumi, lakini badala yake amekuwa akitumia muda mwingi kutafakari safari za nje na namna atakavyoenda kuzungumza huko.

Mutungirehi anamsifu Rais mstaafu Benjamin Mkapa kwa uwezo wake wa kujieleza, na upana wa mawazo anapokuwa anafanya jambo bila kujali kama anasifiwa au la.

Anatabiri kuwa hali hii ikiachwa iendelee maisha ya watu yatakuwa magumu na mfumo wa uzalishaji utasimama, kila mmoja atashindwa kununua wala kuuza.

Wapinzani watamsaidiaje?

Hata hivyo anasema kambi ya upinzani itamsaidia Kikwete kwa kuwaeleza Watanzania matatizo yanayoikabili nchi, ili wachukue hatua, kwani serikali ya sasa haisikilizi matatizo yao. Anawasifu wananchi jinsi walivyoamka na kuwaunga mkono katika harakati zao za kuelekea ukombozi kamili.

Mtungirehi anatoa wito iundwe tume huru ya kuchunguza ufisadi uliuokithiri nchini hadi kufikia hatua wale wanaotuhumiwa kwa ufisadi wakawataja hadharani.

Anasema ikiwa tume huru itaundwa kuchunguza ufisadi na kubaini kuwa walidanganya kwa kutaja watuhumiwa, wao ndio watakaowajibishwa. Anashangaa ni kwa nini serikali haiundi tume hiyo kama madai yao ni ya uongo.

Anamtaka Rais Kikwete aunde tume ya kuchunguza ufisadi huo ili kuonyesha ushupavu na ujasiri hadi nje ya nchi. Na kama angetekeleza hilo tangu zamani watu kama Joseph Butiku wasingeibuka na kuwaunga mkono wapinzani. Anatahadharisha kuwa bila kuunda tume hiyo wapinzani watatangaza mgogoro mkubwa utakaoweza kumwondoa madarakani.

Kuhusu muungano wa vyama, kwanza anakiri kuwa muungano wa ushirikiano wa vyama vinne umewasaidia sana kupata nguvu mpya ya kuweza kulisukuma jahazi la siasa nchini. Anamaliza kwa kutoa wito kwa Watanzania sasa waamke wachunguze mwenendo au uendeshaji wa nchi hii chini ya CCM.

Iwapo watabaini hauwaridhishi kama yeye asivyoamini, wachukue hatua ili kuweza kuing’oa CCM kwa maana kama iking’oka na kukaa pembeni itajifunza kutoka kwa atakayekuwa ameingia madarakani.

Anasema atakayeingia madarakani atakuwa makini kwani atakuwa amejifunza kuanguka kwa CCM. huyo Ndiye Mtungurehi Mwanasiasa Kijana anayelilia Tume ya Uchaguzi amezaliwa wilaya ya Karagwe ni Benedekto Mtungurehi anamke Mmoja na watoto watano.juu