TUWASILIANE KWA E-mail: mobinsons@yahoo.com.

Sunday, February 7, 2010

MATOKEO YA MTIHANI 2009

Na Mwandishi wetu

BARAZA la Mitihani la Taifa limetangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha nne yaliyofanyika Oktoba mwaka jana na kuonyesha namna shule za serikali zilivyoshindwa kufanya vizuri huku idadi ya wadanganyifu katika mtihani huo ikiongezeka.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Joyce Ndalichako, alisema licha ya ongezeko la watahiniwa kwa mwaka jana, idadi ya ufaulu imepungua hasa kwa shule za serikali.

Alisema, julma ya watahiniwa 351,152 walisajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne, kati yao wasichana ni 167,591 sawa na asilimia 47.73 na wavulana 183,561 sawa na asilimia 52.27 wakati mwaka jana watahiniwa 241,472 walisajiliwa.

“Hii inaonyesha idadi ya watahiniwa imeongezeka kwa watahiniwa 109,680 sawa na asilimia 45.42 lakini kwa mwaka jana waliofanya mtihani walikuwa 339,925 sawa na asilimia 96.80 ya waliosajiliwa,” alieleza.

Kuhusu ubora wa ufaulu, Katibu huyo alisema watahiniwa 42,672 sawa na asilimia 17.85 wamefaulu katika daraja la kwanza hadi la tatu ambapo wasichana ni 13,788 sawa na asilimia 12.47 na wavulana 28,884 sawa na asilimia 22.48.

Alisema, watahiniwa waliopata daraja la nne ni 130,651 sawana na asilimia 54.66 wakati waliopata sifuri ni 65,708 sawa na asilimi 27.49 idadi inayoonekana kuongezaka tofauti na mwaka jana.

Akizungumzia hilo, Joyce alisema kati ya shule 10 bora hakuna shule ya serikali hata moja na kueleza kwamba shule zinazoongoza ni zile za seminary na nyingine zinazomilikiwa na watu binafsi.

Katibu huyo alizitaja shule 10 bora zenye watahiniwa zaidi ya 35 kuwa ni shule ya wasichana ya Marian na St. Mary’s Junior Seminary za Bagamoyo, St. James Seminari, Uru Seminari, Anwarite Girls, Maua Seminari na St. Mary Goreti zote za Kilimanjaro. Nyingine ni Don Bosco Seminari ya Iringa, St. Francis Girls ya Mbeya, Feza Boys ya Dar es Salaam,

Aidha, alitaja shule 10 bora zenye wanafunzi chini ya 35 kuwa ni Feza Girls, Thomas More Machrina na Hellen’s za Dar es Salaam, Mafinga Seminari na Bethelsabs Girls za Iringa na St. Joseph-Kilocha seminari ya Kilimanjaro.

Nyingine ni Queen of Apostles Ushirombo ya Shinyanga, Dungunyi Seminar ya Singidai, Rubya Seminari ya Kagera na Sengerema Seminari ya Mwanza.

Alisema nafasi ya kwanza kwa mtahiniwa aliyefanya vizuri imekwenda kwa msichana Imaculate Mosha kutoka Marian Girls wakati mvulana bora ni Gwamaka Njobelo wa shule ya Mzumbe Sekondari.

Hata hivyo alizitaja shule zilizoshika mkia zenye wanafunzi zaidi ya 35 kuwa ni Busi sekondari na Jangalo za Dodoma, Misima, Chekelei na Potwe sekondari za Tanga, Milola na Mandawa za Lindi, Kiwere ya Tabora, Msata ya Pwani na Masanze ya Morogoro.

Sekondari nyingine zilizofanya vibaya zenye wanafunzi chini ya 35 ni Kizara ya Tanga, Mingumbi, Nahukahuka, Marambo, Ruponda na Mpunyule zote za Lindi. Nyingine ni Songolo ya Dodoma, Dole ya Zanzibar, Ruruma ya Singida na Viziwi Njombe ya Iringa.

Pamoja na hayo alisema jumla ya watahiniwa 410 wamefutiwa matokeo yao chini ya kifungu namba 52 cha kanuni za mitihani baada ya kubainika kwamba walifanya udanganyifu.

Aidha, matokeo ya watahiniwa 7,242 yamesitishwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutolipa ada hasa kwa shule za serikali.

Hata hivyo, alisema baraza hilo limetoa onyo kali kwa vituo mbalimbali vilivyobainika kufanya udanganyifu na kuvifutia usajili vituo viwili ambavyo ni Sinza Iteba na Dar es Salaam Prime kwa kukiuka taratibu za uendeshaji wa mitihani.

Mwisho…

No comments: